Shairi
UKWELI Ukweli jama useme, tusikie wanadamu Ukweli usitunyime, tunataka kufahamu Ukweli nausimame, uongo hauna zamu Hata kama ni mchungu, ukweli utakalamu Ukweli kote uvume, Mbeya, Tanga hadi Lamu Ukweli ukawe sime, ya kukata udhalimu Ukweli ukawachome, wote wasojiheshimu Hata kama ni mchungu, ukweli utakalamu Ukweli kama umeme, kwa banati na ghulamu Ukweli usiuzime, twauhitaji kaumu Ukweli bwana Mtume, kasema jambo adhimu Hata kama ni mchungu, ukweli utakalamu Ukweli usiuhame, kwenye wakati mgumu Ukweli kwa mfalme, utaitwa mnajimu Ukweli siumeume, kwa kuhofia mabomu Hata kama ni mchungu, ukweli utakalamu Ukweli ndani ya gome, chungwa likaitwa ndimu Ukweli kwanza upime, utaona umuhimu Ukweli kama kipome, ule haishi hamu Hata kama ni mchungu, ukweli utakalamu Ukweli wake waume, siku hizi ni chandimu Ukweli wa paka shume, unakuja kwa msimu Ukweli huwa kinyume, visipokwepo vitamu Hata kama ni mchungu, ukweli utakalamu Ukweli sote tuseme, waungwana wasalamu Ukweli hapa nikome, na...