Shairi
UKWELI
Ukweli jama useme, tusikie wanadamu
Ukweli usitunyime, tunataka kufahamu
Ukweli nausimame, uongo hauna zamu
Hata kama ni mchungu, ukweli utakalamu
Ukweli kote uvume, Mbeya, Tanga hadi Lamu
Ukweli ukawe sime, ya kukata udhalimu
Ukweli ukawachome, wote wasojiheshimu
Hata kama ni mchungu, ukweli utakalamu
Ukweli kama umeme, kwa banati na ghulamu
Ukweli usiuzime, twauhitaji kaumu
Ukweli bwana Mtume, kasema jambo adhimu
Hata kama ni mchungu, ukweli utakalamu
Ukweli usiuhame, kwenye wakati mgumu
Ukweli kwa mfalme, utaitwa mnajimu
Ukweli siumeume, kwa kuhofia mabomu
Hata kama ni mchungu, ukweli utakalamu
Ukweli ndani ya gome, chungwa likaitwa ndimu
Ukweli kwanza upime, utaona umuhimu
Ukweli kama kipome, ule haishi hamu
Hata kama ni mchungu, ukweli utakalamu
Ukweli wake waume, siku hizi ni chandimu
Ukweli wa paka shume, unakuja kwa msimu
Ukweli huwa kinyume, visipokwepo vitamu
Hata kama ni mchungu, ukweli utakalamu
Ukweli sote tuseme, waungwana wasalamu
Ukweli hapa nikome, naweka chini kalamu
Ukweli usituume, ndungu wawe mahasimu
Hata kama ni mchungu, ukweli utakalamu
Al-husayniy
Mbeya
2022
Comments
Post a Comment