Shairi Hisani ya kizandiki
HISANI YA KIZANDIKI. Tukadhani marafiki, wa kwenye jua na mvua Kushikana kwenye dhiki, pamoja tunakenua Yote haya kumbe feki, tulichelewa kujua WATUGAWIA SAMAKI, SIKUTUFUNZA KUVUA Kugawa wanaafiki, chewa, sato na kibua Kutufunza hawataki, eti tunawasumbua Hawa hawaaminiki, siku watatuzingua WATUGAWIA SAMAKI, SIKUTUFUNZA KUVUA Hisani ya kizandiki, sasa tumeshatambua Katu hawafurahiki, kupiga kwetu hatua Zimefichikana chuki, ndani ya vyao vifua WATUGAWIA SAMAKI, SIKUTUFUNZA KUVUA Tumeshapiga mswaki, kisha tukasukutua Hamna taediriki, fungu lao kuchukua Hata hatutikisiki, tumeshakwisha amua WATUGAWIA SAMAKI, SIKUTUFUNZA KUVUA Waacheni wadhihaki, waseme moto wa bua Tuna mipango lukuki, kichumi kujikwamua Watakuja kuhamaki, nyavu tunavyonunua WATUGAWIA SAMAKI, SIKUTUFUNZA KUVUA Tuunge kile na hiki, tutengeneze mashua Si kazi kutamalaki, mkono aloinua Mola tupe taufiki, mipango iwe murua WATUGAWIA SAMAKI, SIKUTUFUNZA KUVUA...