Shairi Hisani ya kizandiki
HISANI YA KIZANDIKI.
Tukadhani marafiki, wa kwenye jua na mvua
Kushikana kwenye dhiki, pamoja tunakenua
Yote haya kumbe feki, tulichelewa kujua
WATUGAWIA SAMAKI, SIKUTUFUNZA KUVUA
Kugawa wanaafiki, chewa, sato na kibua
Kutufunza hawataki, eti tunawasumbua
Hawa hawaaminiki, siku watatuzingua
WATUGAWIA SAMAKI, SIKUTUFUNZA KUVUA
Hisani ya kizandiki, sasa tumeshatambua
Katu hawafurahiki, kupiga kwetu hatua
Zimefichikana chuki, ndani ya vyao vifua
WATUGAWIA SAMAKI, SIKUTUFUNZA KUVUA
Tumeshapiga mswaki, kisha tukasukutua
Hamna taediriki, fungu lao kuchukua
Hata hatutikisiki, tumeshakwisha amua
WATUGAWIA SAMAKI, SIKUTUFUNZA KUVUA
Waacheni wadhihaki, waseme moto wa bua
Tuna mipango lukuki, kichumi kujikwamua
Watakuja kuhamaki, nyavu tunavyonunua
WATUGAWIA SAMAKI, SIKUTUFUNZA KUVUA
Tuunge kile na hiki, tutengeneze mashua
Si kazi kutamalaki, mkono aloinua
Mola tupe taufiki, mipango iwe murua
WATUGAWIA SAMAKI, SIKUTUFUNZA KUVUA
Tena tutatenda haki, ziwani tunapokua
Hatutorusha fataki, mazingira kuchafua
Mazalia yatabaki, hakuna kuyatibua
WATUGAWIA SAMAKI, SIKUTUFUNZA KUVUA
Beti nane zimetiki, sina budi kupumua
Ya nyongeza siandiki, kalamu nainyanyua
Nipige hapa breki, pasi vumbi kutimua
WATUGAWIA SAMAKI, SIKUTUFUNZA KUVUA
HUSSEIN HUSSEIN
Comments
Post a Comment